Wakulima wakiuza mazao katika soko la Kigoma mjini wengi wakilaumu kushuka bei

Adela Madyane-Kigoma

Kigoma, Tanzania – Wakulima mkoani Kigoma wameendela kupambana na thari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi ambazo zimeathiri msimu wa kilimo ambapo sasa wanategemea kulima msimu mmoja tu badala ya misimu miwili kama ilivyokuwa zamani.

Katika mkoa huo wenye idadi ya watu zaidi ya 2,470,967 kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 zaidi ya asilimia 75 hujishughulisha na kilimo cha mahindi, muhogo, mpunga, maharage na ndizi kama mazao ya chakula na pamba tumbaku kama mazo makuu ya biashara.

Wananchi wa mkoa huo wamekuwa wakiathirika zaidi na misimu ya mvua isiyoeleweka, mara jua, mara mvua, mkoa ambao ulizoea kupata mvua nyingi za vuli mwezi wa tisa na kuanza kupanda mazao yao sasa umekuwa mkoa ambao huanza kuandaa mashamba mwezi huo wa tisa na kuanza kupanda kuanzia mwezi wa kumi.

Akizungumza na Nature News, Bi. Annajesta Paschal mkulima wa Muhogo, wilayani Kibondo alisema pamoja na kwamba muhogo ni zao linalovumilia ukame lakini amekuwa akikutana na changamoto ya wadudu na magonjwa yanayoshambulia muhogo kutoana na upungufu wa mvua

“Nilianza kilimo cha muhogo mwaka 2012, katika kipindi hicho nilipanda muhogo ekari kumi na kuvuna tani za kutosha zilizoniwezesha kupata zaidi ya milioni 50, nilifurahi na kuendelea na kilimo hicho, lakini kwa kipindi kama cha miaka mitano sasa hali imebadilika, napata hasara sana na nimeamua kupunguza ukubwa wa uzalishaji, nimebaki nalima ekari mbili kwaajili ya chakula tu”, alilalamika Pashal

Naye Higwe Cheru mkulima wa mahindi wilayani Kasulu anadai amekuwa akitumia fedha nyingi kwaajili ya kulima kilimo bora cha zao hilo ila kutokana na mvua kutoeleweka amekuwa akipata hasara kinyume na alivyokuwa akifanikiwa kipindi cha nyuma.

“Kilimo cha mahindi kilinipatia nyumba na mashine, watoto wangu walisoma vizuri na sikuwahi kupungukiwa, lakini sasa sielewi, mwanzoni nilidhani nimerogwa kutokana na kupata mazao kidogo lakini sasa naelewa kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi, angalia kama sasa, tumelima na kupanda lakini mpaka sasa si mahindi wala maharage kilichopanda”, alisema Cheru.

Yusta Sanda mkulima wa maharage kutoka Kasulu vijijini alisema yeye huondoka nyumbani kila ifikapo mwezi wa saba na kuweka kambi la kilimo katika eneo la Kagerankanda ambapo hupata mazao zaidi ukilinganisha na anapolimia maeneo karibu na nyumbani

“Hakuna mvua, na zikinyesha zinakuwa za kuharibu mazao, naamua kuondoka kwenda mapori ya Kagerankanda ambapo bado kuna rutuba na angalau tunapata mavuno mazuri, ila hali ya hewa imebadilika kabisa sijui kwa nini”, anahoji Sanda.

Jamii za mwambao wa ziwa Tanganyika nazo zinakutana na changamoto hizo hasa kwa upande wa mafuriko ambayo yalijitokeza kwa miaka ya hivi karibuni 2021-2025 ambayo yalizamisha mashamba ya watu hao na kujikuta wakibaki bila shughuli ya kufanya na kuendelea kuathirika kwa njaa kutokana na uhaba wa chakula.

Yasini Ramadhan mkazi wa Kagera manispaa ya Kigoma Ujiji alisema yeye aliweka nguvu zake katika kilimo mseto eneo la Mgumile ambalo lilikuwa bora kwa mazao ya mchikichi, maharage, mbogamboga na mahindi, lakini mashamba yake yalisombwa na maji yakimuacha asijue cha kufanya kwakuwa maisha yake yalitegemea kilimo pekee.

Akizungumza Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Kigoma, James Peter, alisema kutokana na taarifa zilizotolewa na mamlaka ya hali ya hewa nchini (TMA) mwaka  huu zitakuwa chini ya wastani na wastani, na kwamba mtawanyiko wake hautarajiwi kuwa mzuri.

Peter aliwataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri wa hali hewa na kulima kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo kushauriana nao, sambamba na kutoa taarifa za hatari ili kuhakikisha mkoa unaendelea kuwa na usalama wa chakula na uchumi imara.

Maharage katika soko la mazao Kigoma nchini Tanzania

Akizungumza katika COP 29 aliyekuwa makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango alisema mabadiliko ya tabia nchi yameharibu maisha ya mamilioni ya watu na kuondoa usalama wa chakula na maji safi na salama na kwamba Tanzania inapoteza kati ya asilimia 2 hadi 3 za pato la taifa (GDP) kila mwaka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Ukizungumzia suala hilo, limekuwa moja ya sababu ya udumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ambapo mpaka mwaka 2023 watoto zaidi ya asilimia 27 wa mkoa wa Kigoma walikuwa wanakabiliwa na utapia mlo.

Katika hali hii, ripoti ya Fund for Responding to Loss and Damage (FRLD) kutoka COP30 inasisitiza kuwa ufadhili wa haraka na msaada wa kiufundi ni muhimu kwa jamii zinazokutana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Ana Toni, Mkurugenzi Mtendaji wa COP30, alisema mfuko wa FRLD umefanikiwa kutoa wito wa dola milioni 250 za Marekani kwa ajili ya maombi ya msaada, jambo linaloonyesha kuwa dunia inajiandaa kuhamia kutoka kwenye ahadi za mabadiliko ya tabianchi kwenda kwenye utekelezaji wa haraka.

COP30 imekuwa jukwaa muhimu la kujadili masuala haya, na ripoti za Loss and Damage zinapendekeza kuwa ufadhili wa haraka kwa ajili ya miradi ya kusaidia wakulima, na ufadhili wa kurejesha miundombinu ya kilimo utahitajika ili kuokoa mikoa kama Kigoma.

Serikali ya Tanzania inasisitiza kuwa mchango wa kimataifa kutoka kwa Mfuko wa Loss and Damage (FRLD) unahitajika haraka ili kuhakikisha kuwa mabadiliko haya yanaweza kushughulikiwa.

Kwa sasa, nchi zinazoendelea kama Tanzania zinahitaji msaada wa rasilimali ili kuhakikisha kuwa jamii zinazoathirika na mabadiliko ya tabianchi zinaweza kuhimili changamoto hizi na kutafuta suluhisho la kudumu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here