Cimate change Impact at Ujijii Port in Kigoma Town in Tanzania
Na. Adela Madyane, Nature News, Kigoma
Tanzania imejipanga kuwasilisha ajenda za Afrika katika Mkutano wa 30 wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP30), utakaofanyika Belém, Brazil kuanzia Novemba 10 hadi 21, 2025.
Ikiwa Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN), Tanzania itatumia jukwaa hilo kuongoza mijadala kuhusu haki ya tabianchi, usawa wa kijinsia, nishati safi, na ushiriki wa vijana barani Afrika pamoja na hasara na uharibifu.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Cyprian Luhemeja, amesema kuwa Serikali imezindua Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, inayolenga ustawi jumuishi na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Richard Muyungi, Mwenyekiti wa AGN, amesisitiza kuwa Tanzania itaendeleza msimamo wa Afrika katika kuhakikisha nchi zinazoendelea zinapata msaada wa kifedha na kiufundi unaostahili, hasa kwa jamii zilizo hatarini zaidi.
Wakati huo huo, Mfuko wa Kimataifa wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu (FRLD) umetangaza kuanza kupanga matumizi ya dola za Marekani milioni 250 kwa ajili ya hatua za awali za kusaidia nchi zilizo hatarini zaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Bodi ya FRLD imeidhinisha Mpango wa Utekelezaji wa Barbados (BIM), ambao unalenga kusaidia mbinu zinazoongozwa na nchi na jamii (bottom-up, country-led) ambao unatekelezwa kwa miaka ya 2025 na 2026, na utatoa ruzuku kwa miradi ya kitaifa ya kukabiliana na hasara na uharibifu.
Kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye maendeleo duni (LDCs), inafaidika moja kwa moja na uamuzi wa Bodi kwa kutenga angalau asilimia 50 ya rasilimali za awali kwa ajili ya LDCs na nchi zinazoendelea.
Kufikia Juni 2025, FRLD ilikuwa imepokea ahadi za jumla ya dola milioni 788.8, huku dola milioni 361.0 zikiwa tayari zimewasilishwa na nchi ya Japani ikitajwa kutimiza ahadi yake ya awali kwa kutoa dola milioni 10 kusaidia Sekretarieti ya muda ya FRLD.
Katika kuimarisha uratibu wa fedha za tabianchi, FRLD ilifanya mjadala wa Ngazi ya Juu (HLD) mwezi Aprili 2025 jijini Washington, D.C., uliowakutanisha zaidi ya washiriki 100 kutoka mashirika 44 wito wao ukiwa nchi zilizoendelea zinapaswa kuongeza kasi na wepesi katika kutoa ahadi walizoziweka za kufidia uharibifu na hasara ili kuleta suluhisho katika jamii.
FRLD pia imesaini barua za nia na Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko (Adaptation Fund) pamoja na Mtandao wa Santiago, ili kurahisisha upatikanaji wa msaada wa kifedha na kiufundi.
Mafanikio ya mfuko huu yatategemea uwezo wake wa kuratibu kwa ufanisi na kutoa msaada unaogusa jamii zilizoathirika zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here