Adela Madyane

Tanzania inapoteza zaidi ya shilingi bilioni 500 kila mwaka kutokana na majanga yanayochewa na mabadiliko ya hali ya hewa isiyotabirika huku hifadhi za taifa taifa kama milima ya Mahale ikiathirika zaidi na manadiliko ya tabia nchi.

Ndani ya msimu wa 2024/2025 hifadhi hiyo iliyopo wialaya ya Uvinza ilippoteza idadi kubwa ya watalii na kipato kwa ujumla huku kujaa kwa ziwa Tanganyika kukitajwa kuwa chanzo kikubwa cha athari hiyo ambapo miundombinu muhimu ndani ya hifadhi iliharibiwa.

Kwa mujibu wa mjiolojia wa bonde la Ziwa Tanganyika, Respicius Mshobozi alisema kiwango cha maji kimepanda kutoka mita 776 (mwaka 1976) hadi 776.8 kati ya mwaka 2021–2025 kiwango ambacho kipo karibu sana na rekodi ya juu kabisa ya kihistoria.

Mkuu wa hifadhi ya Milima ya Mahale, Halid Mngofi alithibitisha kwamba licha ya wageni kupungua, pato nalo lilishuka kwa mwaka 2024, na baadhi ya kambi za wawekezaji, ikiwemo kambi ya “Mbalimbali”, zilizama maji.

Barabara ya Mwanga Katubuka Airport Kigoma iliyoharibiwa na mafuriko katika bwawa la Katubuka

Akitoa takwimu za mapato, alisema kwa msimu wa mwaka 2020/2021, idadi ya wageni ilikuwa 210, na hifadhi iliingiza shilingi milioni 180, baadaye idadi ilipanda hadi kufikia wageni 923 mwaka 2024/2025, na kupata shilingi milioni 856.

Hata hivyo, Mngofi alisema kwa msimu wa mwaka 2024 hapakuwa na watalii walioingia kutokana na kambi ya Mbalimbali kufungwa.

Adha mkuu huyo alifafanua zaidi kuwa kupungua kwa watalii hakukuishia tu kwenye kuongezeka kwa kina cha maji  tu bali hata katika usafishaji ambapo barabara ziliharibiwa na mafuriko na kufanya  usafiri wa barabara kuwa mgumu na watalii kusalia katika usafiri wa anga na maji.

Mngofi alieleza kwamba kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, hasa wakati wa msimu wa mvua nyingi, barabara ziliharibika na kuwalazimu wageni kusafiri kwa njia ya ziwa na anga, ambazo huongeza gharama za safari zao.

Alisema hadi sasa, ni wageni wachache wanaosafiri kwa kutumia miundombinu ya barabara kutokana na ukosefu wa barabara inayofika moja kwa moja hifadhini.

Hata hivyo, alisema serikali imejizatiti kukabiliana na athari hizo kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara  kilometa 38 kutoka kata ya Rukoma hadi ilipo hifadhi ya taifa ya milima Mahale

Katika taarifa iliyotolewa na gazeti la Mwananchi mnamo Mei 12, 2023, aliyekuwa Mkuu wa Hifadhi wa Milima ya Mahale, Susuma Kusekwa, alisema Serikali ilitenga shilingi milioni 850 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya kilomita 22 kutoka Buhingu kuelekea katika hifadhi hiyo, kwa kiwango cha changarawe.

Alisema kukamilika kwa barabara hiyo kunatarajiwa kuchangia ongezeko la watalii wanaotumia njia ya barabara.

Kwa mujibu wa Shirika la International Institute for Environment and Development (IIED), mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania yamekuwa tishio kwa maisha ya wananchi, hasa kaya zenye kipato cha chini.

Vilevile ripoti ya tathmini ya hatari ya mwaka 2023 ilionya kuwa mmomonyoko wa pwani, mafuriko, na matukio ya hali ya hewa ya dharura yanatishia usalama wa chakula, afya, na makazi.

Katika muktadha huo huo, Benki ya Dunia kupitia ripoti yake ya Tanzania Country Climate Development Report ilibainisha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanapunguza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuwaathiri zaidi maskini kupitia kupungua kwa mazao, uhaba wa maji, milipuko ya magonjwa, na kupotea kwa rasilimali za uzalishaji.

Tanzania, ikiwa mwanachama wa mikataba ya kimataifa kama UNFCCC, Itifaki ya Kyoto, na Makubaliano ya Paris, imekuwa mstari wa mbele katika majadiliano ya kisera kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Kwa sasa, nchi hii inaongoza Kundi la Afrika (AGN) katika Mkutano wa COP30, ikiwa na dhamira ya kuhakikisha Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu (FRLD) unawanufaisha wananchi wa nchi zilizo hatarini zaidi.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Cyprian Luhemeja, alieleza kuwa ushiriki wa Tanzania katika COP30 ni fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuhamasisha rasilimali fedha, teknolojia bunifu, na uwekezaji wa kijani unaolenga kukabiliana na athari za tabianchi.

 Katika hatua nyingine, Bodi ya FRLD imeanzisha Mfumo wa Utekelezaji wa Barbados (BIM) kwa miaka ya 2025 na 2026, ambapo Dola milioni 250 zimetengwa kwa ajili ya ruzuku kwa nchi zilizo hatarini. Tanzania, ikiwa miongoni mwa nchi 44 zinazoendelea zaidi (LDCs), inastahili kupata angalau asilimia 50 ya mgao wa rasilimali hizo.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 imeweka vipaumbele vya kujenga uchumi shindani wa kijani, ustawi jumuishi, na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi. Kauli mbiu ya “Utekelezaji wa Hatua Jumuishi za Ustahimilivu wa Tabianchi” inasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, jamii, na wadau wa maendeleo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here