Adela Madyane – Kigoma
Wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zikiendelea kuvuruga mfumo wa maisha ya wananchi nchini tanzania kwa kusababisha mabadiliko katika mifumo ya hali ya hewa hasa mvua, kutokea kwa ukame, kukosekana kwa nishati na majanga mengine, mkazi wa kijiji cha Simbo katika halmashauri ya wilaya ya Kigoma, Hassan Kilanoza, ameibuka kama mfano wa ubunifu unaotumia rasilimali zilizopuuzwa kuokoa mazingira na kuboresha maisha ya jamii.
Kilanoza, anayejihusisha na uchakataji wa mkaa banifu na uzalishaji wa gesi inayotokana na taka mbalimbali (biogas) kwa kutumia mabaki ya zao la mchikichi ikiwa ni kufanyia kazi wito wa Umoja wa mataifa wa kila nchi kutumia rasilimali asilia katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo ni matokeo ya ukataji miti kihorela, uchafuzi wa mazingira na kilimo katika vyanzo vya maji kinachosababisha kukauka kwa mito na uzalishaji mkubwa wa hewa ukaa kutokana na uchafuzi wa mazingira, uchomaji moto misitu

Akizungumza na mwandishi wa habari za mazingira kutoka taasisi ya Natrure Tanzania katika kiwanda chake kijijini hapo, Kilanoza alisema hutumia kila sehemu ya zao la mchikichi ikiwemo matunda ya mchikichi yanayofahamika kwa jina la “ngazi” kwa mujibu wa wenyeji, ambayo baada ya kuchakatwa hutoa mawese, makapi, mise na maji machafu maarufu kama mnyemwe.
Anasema amekuwa akifuatilia taarifa mbalimbali za kisanyansi na kimazingira kuhusu changamioto za mabadiliko ya hali ya hewa na wito wa umoja wa mataifa kukabiliana na uhaba wa nishati, maji na ongezeko la hewa ukaa na kubaini kuwa makapi na taka nyingine zinazotokana na viwanda vya uchakataji wa zao la michikichi ni suluhisho sahihi kwa mazingira
Anabainisha kuwa mise hutumika kutengeneza mafuta ya kupikia na sabuni za kienyeji maarufu kama sabuni za Kigoma, huku maganda yakitumika kama kuni.
Aidha, ameamua kutumia maganda hayo pamoja na taka nyingine ngumu na kavu kuzalisha mkaa banifu rafiki kwa mazingira.
“Katika zao la mchikichi hakuna kinachopotea, kila kitu kina faida kinachohitajika ni maarifa na mtaji,” anasema Kilanoza.
Kwa upande wa gesi, anasema hutumia maji machafu yanayotokana na uchakataji wa mawese kuzalisha biogas kwa matumizi ya kupikia, hatua aliyosema imepunguza uchafuzi wa mazingira na utegemezi wa kuni.
Anaongeza kuwa katika eneo analofanyia kazi kuna zaidi ya mashine 60 za kuchakata mchikichi zinazozalisha taka nyingi ikiwemo mapangasuli na mnyemwe, ambapo huzikusanya na kuzitumia kuzalisha nishati mbadala.
“Taka hizi zilikuwa zinatoa harufu mbaya na kuharibu mazingira, lakini sasa zimekuwa rasilimali, nalinda mazingira na kupata kipato,” anasema Kilanoza
Anasema ana uwezo wa kuzalisha hadi tani 10 za mkaa banifu kwa siku, huku mkaa huo ukidumu zaidi ya saa 12 bila kuzimika, hautoi moshi na huuzwa kwa shilingi 400 kwa kilo, bei inayoweza kumudu wananchi wengi.
Kilanoza anasema wazo la mradi huo lilitokana na mafunzo aliyopata kutoka Catholic Relief Services (CRS) walipomchagua kuwa mkufunzi wa utengenezaji wa biogas, jambo lililompa maarifa ya kubadili taka kuwa fursa ya kiuchumi.
Manufaa katika mazingira
Kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira, gunia moja la mkaa lenye uzito wa kilo 100 huzalishwa kwa kukata miti kati ya mitatu hadi mitano.
Hii ina maana kuwa ili kupata tani 10 za mkaa sawa na kilo 100,000 au magunia 100, kunahitajika kukatwa miti kati ya 300 hadi 500.
Kwa wastani, hekta moja hupandwa miti kati ya 400 hadi 600. Hivyo uzalishaji wa tani 10 za mkaa wa kawaida husababisha ukataji wa zaidi ya hekta moja ya misitu.
Kwa muktadha huo, tani 10 za mkaa banifu zinazozalishwa na Kilanoza kwa siku huokoa zaidi ya hekta moja ya misitu ambayo ingekatwa kwa ajili ya kuni na mkaa wa kawaida, hatua inayochangia uhifadhi wa mazingira na kupunguza uharibifu wa misitu.
Utekelezaji wa sheria na makubaliano ya kimataifa
Kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ya Paris Agreement ya mwaka 2015, yaliyofikiwa chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), nchi wanachama zilikubaliana kupunguza uzalishaji wa hewa chafu kwa kudhibiti ukataji miti na kukuza matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.
Hatua hizo pia zinaendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu namba saba yanayolenga kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi na nafuu.
Aidha, Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2022 inasisitiza uhifadhi wa misitu ya asili, matumizi ya nishati mbadala na kupunguza utegemezi wa mkaa unaotokana na miti, huku ikiihimiza jamii na sekta binafsi kushiriki katika uhifadhi wa misitu.
Katika muktadha huo, ubunifu wa Kilanoza wa kutumia mabaki ya kilimo kuzalisha nishati mbadala unaonekana kuwa sehemu ya suluhisho la uchafuzi wa mazingira na utegemezi wa mkaa wa miti ya asili.
Msaada wa Serikali na wadau wa maendeleo
Afisa mazingira wa halmashauri ya wilaya ya Kigoma, Noseth Mdunya, anasema walimtambua Kilanoza na kumunganisha na CRS ili kuimarisha juhudi za kulinda mazingira kupitia uchumi rejeshi.
Alisema juhudi zake zimekuwa mfano kwa wakulima na wachakataji wengine wa mchikichi katika halmashauri hiyo ambako zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wanategemea zao hilo.
Kwa upande wake, afisa biashara wa halmashauri hiyo, Immaculatha Kipeta, alisema mjasiriamali huyo ameunganishwa na SIDO kwa ajili ya kuboresha ubora wa bidhaa na kukuza biashara.
Afisa kilimo wa wilaya hiyo, Ramadhan Mpasiwakomu, anasema serikali inaendelea kumtafutia fursa za kifedha kupitia taasisi mbalimbali ikiwemo Benki ya Kilimo.
Naye afisa maendeleo wa wilaya hiyo, George Vangesauli, anasema kuna mpango wa kumpeleka katika maonesho ya Sabasaba ili kujifunza na kuongeza ubunifu.
Afisa mwandamizi wa mradi wa VOICES kutoka CRS, Simon Mwanjera, anasema mradi huo unalenga kukuza uchumi rejeshi kwa kubadili taka kuwa fursa, kulinda mazingira na vyanzo vya maji ikiwemo kuboresha maji ya Ziwa Tanganyika.
Anasema kupitia mradi huo Kilanoza ataendelea kunufaika na fursa mbalimbali ikiwemo kupatiwa mafunzo zaidi sambamba na fedha za ruzuku ili kukuza mtaji wake
Mafanikio
Kilanoza alisema amekuwa akifanya shughuli hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja na mafanikio yake ni pamoja na kuinuka kiuchumi na kuwafundisha vijana kutengeneza mkaa mbadala na biogas, ambapo hulipa ada ya shilingi 50,000 kupata mafunzo.

Changamoto
kukosekana kwa uungwaji mkono katika bunifu mbalimbali kwenye sekta ya mazingira ni ombwe linaloshusha hamasa kwa jamii hususani vijana kujihusisha na bunifu za kimazingira.
Bunifu katika uhifadhi ni njia moja wapo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi hasa kwa jamii kutumia rasilimali zinazowazunguka kubuni zana au bidhaa zenye uwezo wa kubadili taka kuwa nyenzo mahususi za kuwezesha kuwepo kwa matumizi mbadala wa bidhaa zilizokwisha kutumika au matumizi ya mazingira kwa mfumo endelevu.
Licha ya mafanikio hayo yanayotajwa na Bw. Kilanoza, alisema bado anakabiliwa na changamoto ya mtaji ili kuongeza uzalishaji. Alisema anahitaji mashine zaidi na gari kwa ajili ya ukusanyaji wa taka na usambazaji wa bidhaa, akieleza kuwa mashine moja hugharimu zaidi ya shilingi milioni 10.
“Nahitaji mtaji wa kukusanya taka na kusambaza bidhaa. Kwa sasa nina mashine moja inayozalisha tani 10 kwa siku, lakini siwezi kupokea tenda kubwa kwa sababu ya ukosefu wa usafiri,” alisema.
Aliongeza kuwa ili kuongeza uzalishaji hulazimika kuuza kwanza mkaa waliotengeneza ili kupata fedha za kuzalisha mwingine, hali inayochelewesha ukuaji wa biashara.
Kilanoza pia alieleza changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara hali inayokwamisha shughuli za uchakataji.
Maoni ya wadau
Mnunuzi wa mkaa mbadala, Jummane Nziganije, alisema mkaa huo ni bora na rafiki kwa mazingira, akiiomba Serikali kuwawezesha wabunifu wa ndani.
“Bila kuwawezesha wabunifu kama Kilanoza, vita dhidi ya uharibifu wa mazingira itakuwa ngumu,” alisema.
Kwa mujibu wa takwimu za setilaiti kutoka Global Forest Watch, kati ya mwaka 2001 na 2023 Tanzania imepoteza zaidi ya hekta milioni mbili za misitu, jambo linaloonesha umuhimu wa ubunifu wa nishati mbadala katika kulinda mazingira.




