Alliance one yapongezwa kwa mchango wake katika upandaji wa miti mkoani Kigoma

Kampuni ya tumbaku ya Alliance One Tanzania Tobacco Limited imepongezwa kwa kutoa mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira mkoani Kigoma kupitia katika miradi ya kurejesha uoto wa miti katika maeneo yaliyoathiriwa na shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabia nchi.

Pongezi hizo zimetolewa na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2026 Bw. Wazo Mwang’onda baada ya kukagua mradi wa shamba la miti katika shule ya sekondari Muganasha wilayani Buhigwe linalofadhiliwa na kamuni hiyo

Bw. Mwang’onda amebainisha kuwa kitendo cha kampuni ya Alliance One kuamua kuwekeza katika upandaji wa miti ni cha kizalendo na chenye nia ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhifadhi mazingira na kukuza Uchumi wa wananchi kupitia kilimo cha tumbaku na miti.

Mwang’onda ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Alliance One kuendelea kutoa usaidizi wa ujuzi kwa halmshauri za wilaya mkoani Kigoma pamoja na kuwajengea uwezo wananchi ili nao waanzishe mashamba yao na kukabailiana na jangwa ambalo linadhihirika kwa maeneo omengi ya wilaya ya Buhigwe kutokuwa na miti huku ardhi ya wilaya hiyo ikiruhusu kilimo cha miti yam bao na mataunda

“Nawapongeza kampuni ya Alliance One kwa juhudi kubwa mnayofanya katika mikoa mingi nchini Tanzania kwa kuanzisha na kuendeleza mashamba ya miti ikiwa ni sambamba na kuwapa hamasa na ujuzi wananchi katika sekita ya kilimo na mazingira, wito wangu kwenu sasa anzeni kuwahamasisha na kuwafundisha wananchi kupanda miti ya matunda hususani Parachichi ili pamoja na kuwapa kuni wapate matunda ambayo sasa yana soko kubwa kimataifa” Alisisitiza Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Wazo Mwang’onda

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2026 Ndg. Wazo Mwang’onda akizungumza baada ya kukagua na kuzindua shamba ya miti linaloratibiwa na kampuni ya Tumbaku ya Alliance One Tobacco Tanzania Limited, katika kijiji cha Songambele wilayani Buhigwe mkoa wa Kigoma

Mwang’onda amesisitiza kuwa ardhi ya wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma inafanana na maeneo mengi ya mkoa wa Njombe na Ruvuma ambako pamoja na kupanda miti yam bao, wananchi wamehamasishwa kuanzisha mashamba makubwa ya Parachichi na wakulima walioitikia wito huo sasa Uchumi wao unakuwa kutokana na biashara ya mbao na matunda

Kitoa taarifa ya miradi shirikishi ya mazingira inayotekelezwa na kampuni ya Alliance One, Meneja wa Kanda ya magharibi Bw. Salum Rashid amesema Mpango huo ulianza katika Mwaka wa Kilimo 2022/23 huko Ngukumo, Nzega, mkoani Tabora na baadaye Kasulu na Buhigwe mkoani Kigoma katika Mwaka wa Kilimo 2024.

Amebainisha kuwa utekelezaji wa miradi ya uoteshaji na upandaji wa miti huanza kwa kusaini makubaliano kati ya AOTTL na mmiliki wa ardhi aliye tayari kushiriki katika uanzishaji wa shamba la miti, kwa lengo la kutoa nishati endelevu kwa wakulima wa tumbaku.

Tangu mwaka 2024 hadi sasa, kampuni imeanzisha shamba la miti lenye ukubwa wa hekta 966 sawa na takriban miti 2,415,675 katika Mkoa wa Kigoma kati ya hiyo, hekta 414 zimepandwa katika eneo la wilaya ya Buhigwe, zikiwakilisha miti 1,035,000.

Kwa upande wake Mratibu wa shughuli za Alliance One mkoani Kigoma Bw. Robert Mogella ameweka bayana kuwa gharama za uendeshaji kwa ajili ya kusimamia hekta 414zilizopandwa katika eneo la shule ya sekondari Muganasha katika kijiji cha Songambele kwa kipindi cha miaka miwili ya kilimo ni TZS 1,264,723,200.

Baadhi ya wafanyakazi na maafisa mazingira wa kampuni ya Alliance One Tanzania Tobacco Limited mkoani wa Kigoma

Bw. Mogella ameeleza kuwa pamoja na malengo mengine ya kukabiliana matumizi ya misitu asilia kwa ajili ya kuni za kukaushia tumbaku, kampuni hiyo ina malengo ya kuhamasisha jamii kuwekeza katika upandaji miti kwenye ardhi iliyoharibika ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mkuu wa wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Kanali Michael Ngayalina akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa amebainisha kuwa Kampui ya Alliance One (AOTTL) imetoa mchango mkubwa kwa serikali na imekuwa chachu kwa wananchi kuanza kuthamini ardhi iliyokuwa imetelekezwa na sasa jamii inapanda miti katika mashamba yao.

Naye afisa Mazingira wa wilaya hiyo Bi. Asha Athuman Luhuiy ameweka bayana kuwa AOTTL ni mdau mhimu katika sekta ya mazingira wilayani Buhigwe na kwamba kampuni hiyo imeiwwezesha wilaya kuvuka lengo la upandaji miti milioni moja na laki tano kwa mwaka

Mwenge wa Uhuru umeanza mbio zake leo Septemba 11, 2026 katika Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, ukitokea Wilaya ya Kasulu, ambapo unatarajiwa kuzindua, kutembelea, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akisoma taarifa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Mganasha wilayani Buhigwe, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Michael Ngayalina, amesema Mwenge huo utakimbizwa umbali wa kilomita 54 na kuzindua na kutembelea jumla ya miradi 7 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 15.4 ikiwemo inayosimamiwa na Kampui ya Alliance One Tobacco Tanzania Limited

Mwaka 2025 pia Mwenge wa Uhuru ulitembelea na kukagua shamba la miti ya Alliance One katika eneo la Buhigwe mkoani Kigoma ambalo lilitolewa na kikundi cha wakulima walioona fursa ya upandaji miti kama nyenzo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.

Kwa sasa wamiliki wengi wa misitu wananufaika na biashara ya magogo ambayo huuzwa na kusafirishwa kwenda katika mikoa ya Geita, Shinyanga na Mwanza kwa ajili ya shughuli za migodi ya madini

 

Leave a Reply