Adela Madyane, The Nature News -Kigoma
Kufuatia wito wa kupata msaada kutoka Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu unaotokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi (FRLD) kuanzia mwezi Disemba kwa nchi zinazoendela, Tanzania imeitaka bodi ya FRLD kuhakikisha upatikanaji wa fedha unakuwa wa wazi, haki na endelevu.
Akizungumza katika mkutano wa umoja wa mataifabwa mabadiliko ya tabia nchi (COP30) huko Balem, mwenyekiti wa wa kikundi cha Majadiliano cha Afrika (AGN) Dkt. Richard Muyungi ambaye pia mshauri wa Rais kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi nchini alisema mafanikio ya FRLD yanategemea uwazi na kasi ya utoaji wa fedha.
“Fedha lazima ziwe zenye uthabiti na zipatikane kwa wakati, mfuko huu hauwezi kuwa wa majaribio kwasababu linagusa maisha ya watu,” amesema Dkt. Muyungi.
Amesisitiza kuwa Fedha hizo zinalenga kushughulikia hasara mbalimbali, kuanzia miundombinu iliyoharibika hadi kupotea kwa urithi wa kitamaduni ulisababishwa na mabadiliko ya tabianchi yanayotabirika na endelevu.
Kutokana na umhimu wa kutenmgwa kwa fedha kwa ajili ya mfuko huo, Dola milioni 250 zimetengwa kwa ajili ya hasara na uharibifu kwa nchi zinazoendelea Tanzania kupata zaidi dola milioni 20
Dr. Muyungi aliliambia the Nature News Tanzania kuwa tatizo kubwa lililopo ni urasimu unaochelewesha upatikanaji wa fedha, ambapo nchi masikini mara nyingi hazina uwezo wa kitaasisi kushughulika na mifumo migumu ya kimataifa na kuwa tunahitaji njia rahisi na msaada wa kiufundi ili fedha hizi ziwafikie walio mstari wa mbele.
Muyungi alifafanua zaidi kuwa mafanikio ya wito huo wa kwanza wa maombi ya ufadhili chini ya Mpango wa Utekelezaji wa Barbados (BIM), yatapimwa kwa kasi na usawa wa jinsi unavyosaidia mataifa yaliyoathirika zaidi na majanga ya tabianchi.
Aidha Dkt Muyungi alisema Tanzania inatarajia kunufaika na kiasi cha fedha hadi dola milioni 20 kwa kila mradi ulioathirika na unahitaji utekelezaji wa kukabiliana na athari za mabadiliko hayo.
“Nasisitiza huu sio mkopo ni ufadhili, na hadi sasa tuna mambo ya kufuatilia na sisi kama nchi ili tumepewa kipaumbele hivyo tunaweza kuwa na miradi hata miwili ambayo inaweza kuwa na manufaa makubwa, naomba ofisi ya makamu wa Rais tuteue mtu mmoja yaani focal person kwaajili ya mfuko wa kukabiliana n Hasara na Uharibifu” Alisema
Dkt Muyungi aliwaomba Watanzania kutoka serikalini na sekta binafsi wanaoshiriki katika mkutano huo wenye takribani washiriki 60,00 kusimama kama nchi na kujenga mitandao ya kuchangamkia fursa ili kuendelea kuinufaisha nchi.Baada ya kuidhinishwa kwa Mpango wa Barbados, Bodi ya FRLD imeanza kazi rasmi kwa kutenga dola milioni 250 za Marekani (takriban Sh612.6 bilioni) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya mwaka 2025–2026.
Kwa upande wa mkurugenzi wa Mtandao wa Kiraia wa Haki za Tabianchi (CAN Tanzania), Pendo Mwakisimba, alisema COP30 ni fursa ya kihistoria kwa dunia kugeuza ahadi za fedha kuwa vitendo.
“Kuna pengo kubwa kati ya maneno na fedha, dunia inatoa ahadi za mabilioni, lakini kinachofika ni kidogo mno,” amesema.
Kwa mujibu wa CAN, wakati nchi zinazoendelea zinahitaji dola za marekani bilioni 387 sawa na shilingi Trilioni 1,006.2 kila mwaka hadi mwaka 2030, fedha zilizotolewa mwaka 2022 zilikuwa dola bilioni 27.5 sawa na shilingi trilioni 71.5 pekee, kiasi ambacho ni kidogo mno.
“Hilo ndilo linaloitwa pengo la haki za tabianchi, walioteseka zaidi wanapata kidogo zaidi,” alisema Mwakisimba
Ushiriki wa Tanzania unaoongozwa na ujumbe wa ngazi ya juu unaonesha dhamira ya taifa katika kukabiliana na janga la tabianchi na nafasi yake ya kimkakati ndani ya Kundi la Majadiliano la Afrika.
Vipaumbele vya Tanzania katika mkutano huu unaoendelea ni pamoja na kuhakikisha mfuko wa FRLD unafanya kazi kikamilifu kwa ufadhili wa uhakika, kuendeleza utekelezaji wa Mipango ya Kitaifa ya Urekebishaji (NAPs), na kuhamasisha fedha za kutosha kwa nchi zinazoendelea.
Matarajio ya wananchi waliothirika ni kuona fedha hizo zinafika katika maeneo yaliyoathirika zaidi hasa kwa kuzingatia wananchi wanaoishi katika hali ya umaskini waliothirika.




